Na. Shinyanga RS
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Shinyanga na kuagiza ifikapo tarehe 11 Oktoba, 2023 kuwa limekamilika kwa awamu ya kwanza ambayo ni milango iliyopo ghorofa ya chini.
Mhe. Mndeme ameyasema hayo leo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa soko hilo, kuongea na wafanyabiashara, kusikiliza kero zao na kuzitatua ambapo pamoja na mambo mengine pia ameziagiza Halmashauri zote Mkoani Shinyanga kuhakikisha wanatenga chumba maalum ambacho kitatumika na wafanyabiashara wanawake wenye watoto ili waweze kuwanyonyesha watoto wao na kuwa sehemu sahihi kwa watoto hao kucheza wakati wazazi wao wakiwa katika biashara.
"Siwezi kusema nimeridhishwa, hapana niseme tu kwamba sijaridhishwa kabisa na kasi ya ujenzi wa soko hili, niwaagize kufikia tarehe 11 Oktoba, 2023 ujenzi wa vyumba ghorofa ya chini uwe umekamilika ili wafanyabiashara waanze kazi zao haraka wapate kipato, na serikali ipate pato lake," alisema Mhe. Mndeme.
Ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Shinyanga wenye vyumba vya biashara 106 utagharimu Tzs. Bilioni 1.8 fedha kutoka mapato ya ndani ya Manispaa yatokanayo na makusanyo, ambapo mpaka sasa ni asilimia 56 ya ujenzi wote imekwishatekelezwa huku asilimia inayobakia inatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 11, 2023.
Baadhi ya picha zikionesha Mhe. Christina Mndeme akiwa katika soko kuu la manispaa ya shinyanga wakati wa alipotembelea kukagua, kuongea na wafanyabiashara, kusikiliza na kutatua kero zao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa